HUKU sakata la mirathi ya marehemu Steven Charles Kanumba aliyekuwa
gwiji wa filamu Bongo, likiendelea kufukuta chini kwa chini, baba mzazi
mzee Charles Kusekwa Kanumba amegawanya mali za mwanaye, Risasi
Mchanganyiko linakufunulia.
Mali za marehemu Kanumba zinazotajwa
katika mgawo huo ni pamoja na kampuni yake iitwayo Kanumba The Great
Film Company na magari.
HABARI KAMILI
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka
Shinyanga, mzee Kusekwa (pichani) alisema yeye kama baba wa marehemu ana
jukumu la kuwa msimamizi wa mirathi na kugawa mali za mwanaye.
“Tumekaa huku Shinyanga na ndugu wengine, hili suala la mirathi
linapaswa kuwa chini yangu kwa sababu mimi ndiye baba. Kimila za kikwetu
(Kisukuma), msimamizi wa mirathi huwa ni baba,” alisema mzee Kusekwa.
Akaongoza: “Kutokana na hilo, nimechukua jukumu la kugawa mali za
marehemu mwanangu kwa kuzingatia usawa, haki na vigezo muhimu.”
MGAWANYO WENYEWE
Katika mgawo huo, mzee Kusekwa alitaja sehemu za mali za marehemu Kanumba huku akiacha nyingine.
Mali ambazo hakuzitaja na zinajulikana ni pamoja na akaunti za benki,
viwanja viwili vilivyopo Mbezi, Msakuzi nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam pamoja na mali nyingine.
Aliwataja mama mzazi wa marehemu,
Flora Mtegoa, mdogo wa Kanumba aliyekuwa akifanya naye kazi kwa karibu
enzi za uhai wake, Seth Bosco.
Alisema, katika mgawo huo yeye kama
baba anastahili kuchukua gari la kifahari alilokuwa akitumia mwanaye
wakati wa uhai wake, aina ya Toyota Lexus na Bi. Mtegoa achukue gari
ndogo aina ya Toyota GX 110.
“Ile kampuni ya filamu (Kanumba The Great Film Company) watachukua Seth na dada yake,” alisema mzee Kusekwa.
Kwa sasa, wanaosimamia kampuni hiyo iliyopo Sinza, Mori, jirani na Baa
ya Meeda jijini Dar es Salaam ni Seth na dada yake aitwaye Bela.
MPANGO WAKWAMA
Wakati hayo yakiendelea, ilielezwa kuwa mzazi huyo
alituma wawakilishi wake kutoka Shinyanga hadi jijini Dar kwa lengo la
kufungua mirathi.
Habari za ndani kutoka kwa chanzo chetu makini
ambacho hakikupenda jina litajwe gazetini, zinasema kwamba wawakilishi
hao walifika katika Mahakama ya Mwanzo ya Kinondoni lakini walikwama.
“Hawafanikiwa kufungua mirathi maana hawakuwa na vielelezo vya kutosha.
Walitakiwa kuwa na cheti cha kuzaliwa na cha kifo cha Kanumba pamoja na
vielelezo vingine ambavyo hawakuwa navyo,” kilisema chanzo hicho na
kuongeza:
“Basi baada ya kukwama, hawakuwa na la kufanya zaidi ya kurudi Shinyanga.”
MAMA KANUMBA
Mama wa marehemu Kanumba, Bi. Mtegoa alipoulizwa
anachofahamu kuhusu ujio wa wawakilishi wa mzazi mwenzake alisema:
“Nilisikia wamekuja, lakini sijapata kuwaona kabisa. Tumesubiri mpaka
sasa kuona kama tutaitwa mahakamani lakini hatujaitwa.”
Akaongeza:
“Kiukweli sijui nini kimetokea, maana siku chache baada ya arobaini ya
mwanangu, tuliweka kikao hapa Dar na mwenzangu (baba Kanumba) alituma
watu wawili waliokuja kumuwakilisha.
“Baada ya makubaliano hayo,
tuliwekeana sahihi wanandugu wa pande zote mbili na hata baba Kanumba
alikubaliana na watoto wake waliokuja kumuwakilisha kuhusu uteuzi
huo...sasa haya tena yananishangaza maana hata mahakamani kufungua
mirathi bado sijaenda.”
Latest News!
Advertisement
Related Posts
Leave a reply
0 comments for "Mali za Kanumba zagawiwa"